Kwa mujibu wa Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji, Imamu wa Ijumaa wa Najaf, katika khutba za Swala ya Ijumaa alizozitoa katika Husseiniyya Kuu ya Fatimiyya mjini Najaf, alieleza mitazamo yake kuhusu masuala muhimu ya Iraq na eneo.
Tunatoa Wito wa Umoja wa Umma wa Kiislamu, Shia na Sunni, pamoja na Madhehebu na Makabila Yao Yote
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji alisema: Tuko katika siku za maadhimisho ya kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Mtukufu (s.a.w.w.), na Qur'ani inasema:
﴿وَإِنَّ هَٰذِهِ أُمَّتُکُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً﴾
“Na hakika Umma wenu huu ni Umma mmoja.”
Tunapaswa kujiepusha na msimamo au kauli yoyote inayochochea fitna za kimadhehebu, kwa sababu:
﴿الْفِتْنَةُ أَشَدُّ مِنَ الْقَتْلِ﴾
“Fitina ni mbaya zaidi kuliko kuua.”
Tunatoa wito wa umoja wa Umma wa Kiislamu, Shia na Sunni, pamoja na madhehebu na makabila yao yote; tukitekeleza kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu isemayo:
﴿وَإِنَّ هَذِهِ أُمَّتُکُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّکُمْ فَاتَّقُونِ﴾
“Na hakika Umma wenu huu ni Umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu, basi nicheni.”
Na katika aya nyingine:
﴿إِنَّ هَٰذِهِ أُمَّتُکُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّکُمْ فَاعْبُدُونِ﴾
“Kwa hakika Umma wenu huu ni Umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu, basi niabuduni.”
Si jambo linaloruhusiwa kutamka kauli yoyote inayosababisha chuki na uadui kati ya makabila na madhehebu ya Kiislamu.
Urafiki kati Yetu na Iran ni wa Pande Mbili katika Ngazi Zote, Hivyo Shukrani kati ya Mataifa Mawili Nazo ni za Pande Mbili
Katika sehemu nyingine ya khutba yake alisema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilituma ujumbe nchini Iraq kwa niaba ya Uongozi Mkuu wa Mapinduzi, ili pamoja na kukutana na viongozi wakuu wa Iraq, kutoa shukrani kwa niaba ya uongozi wa Iran kwa wananchi wa Iraq kutokana na misimamo yao kuhusu Jamhuri ya Kiislamu.
Sisi pia, kwa upande wetu, tunaishukuru Jamhuri ya Kiislamu, na hatutasahau kuthamini misimamo yao katika kuhakikisha upatikanaji wa gesi Iraq, pamoja na msimamo wao kuhusu uuzaji nje wa mafuta ya Iraq kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz; kwa hiyo, shukrani kati ya mataifa haya mawili ni za pande zote.
Suala la Ukiritimba wa Silaha Linapaswa Kutatuliwa kwa Moyo wa Mapenzi na kwa Kupata Mwongozo kutoka kwa Marja'iyya ya Kidini
Katika sehemu nyingine kuhusu masuala ya ndani, alisema: Tunakaribisha wito wa kutafuta suluhisho la amani kuhusu suala la ukiritimba wa silaha, na suala hili linapaswa kutatuliwa kwa moyo wa mapenzi kati ya serikali na makundi ya Muqawama, na kabla ya hapo liambatane na kuomba mwongozo kutoka katika mtazamo wa Marja'iyya ya kidini na kuondolewa kambi za kijeshi za Marekani nchini Iraq.
Onyo kwa Saudi Arabia Kuhusu Kuitambua Israel na Kurejesha Mahusiano ya Kawaida Nayo
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji, kuhusu masuala ya kimataifa, alisema kwa msisitizo: Tunauonya Ufalme wa Saudi Arabia kuhusu kuitambua Israel na kurejesha mahusiano ya kawaida nayo.
Trump ameweka sharti la kuitambua Israel ili Marekani ikubali makubaliano ya nyuklia kati ya Marekani na Saudi Arabia.
Tunaamini kwamba Saudi Arabia, ambayo ni chimbuko la Kaaba Tukufu na Haramu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.), inapaswa kuitunza ardhi yake ikiwa safi kutokana na aina yoyote ya kurejesha mahusiano ya kawaida na utawala wa Kinyang'anyi.
Pia alisema kuhusu masuala ya kimataifa: Muungano kati ya Pakistan na Kuwait katika makubaliano ya kiusalama, na kabla yake katika wiki zilizopita muungano kati ya Uturuki, Pakistan na Saudi Arabia, unaonyesha kwamba nchi hizi zinahisi kuwa madola ya kibeberu hayana uwezo wa kuzilinda.
Kwa hiyo, zinapaswa kujihakikishia usalama wao wenyewe kwa uwezo wao wa ndani, na ahadi ambazo madola makubwa yamezitoa si za kweli tena; kwa sababu wote tunashuhudia kuwepo kwa pengo la kiusalama ambalo linapaswa kuzibwa kwa ulinzi wa ndani na wa kujitegemea miongoni mwao.
Khutba ya Kidini
Mhubiri wa Ijumaa wa Najaf Tukufu, baada ya kutoa ushauri wa kumcha Mwenyezi Mungu, alisema: Tuko katika siku za maadhimisho ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu (s.a.w.w.), na katika mnasaba huu inafaa tukumbushe baadhi ya mambo kuhusu Utume wake:
Kwanza: Ulimwengu mzima wa Uislamu, kwa sababu Uislamu na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) walitumwa kwa ajili ya walimwengu wote:
﴿وَمَا أَرْسَلْنَاکَ إِلَّا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِینَ﴾
“Na hatukukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu.”
Pili: Kuhitimishwa kwa Utume kwa Uislamu, kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) ndiye Mwisho wa Manabii; hakuna Utume wala Sheria isipokuwa Sheria ya Mwenyezi Mungu na Sheria ya Bwana wa Mitume inayoweza kuwaokoa wanadamu.
Aliendelea kusema: Tatu: Kwamba Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) ni rehema kwa walimwengu, kutokana na fadhila na neema ambayo Mwenyezi Mungu ametuteremshia; kwa hiyo Mwenyezi Mungu anasema:
﴿لَقَدْ مَنَّ اللَّهُ عَلَی الْمُؤْمِنِینَ إِذْ بَعَثَ فِیهِمْ رَسُولًا مِّنْ أَنفُسِهِمْ﴾
“Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewafanyia waumini neema alipowatuma miongoni mwao Mtume kutoka miongoni mwao wenyewe.”
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na Mtukufu, kwa wema huu wa Kimungu.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji, mwishoni, alisema: Kile ambacho Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) alikitabiri kuhusu ulimwengu kurejea katika Uislamu, aliposema:
(لا تقوم الساعة حتی یخرج رجل من ولدی یملأ الأرض قسطاً وعدلاً بعدما ملئت ظلماً وجوراً)
“Qiyama hakitasimama mpaka atoke mtu miongoni mwa kizazi changu, ambaye ataijaza dunia kwa uadilifu na haki, kama ilivyojaa dhuluma na uonevu.”
Kwa hiyo, leo tunasubiri kuenea kwa Uislamu duniani kote kupitia mikono ya Imam wa Zama (ajil-Allahu ta'ala farajahu sharif).
Na katika maadhimisho ya kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume wetu (s.a.w.w.), pia inafaa niwasomeeni nasaha na wasia wake.
Maoni yako